Rais Jakaya Mrisho Kikwete (yumo garini kushoto) akikagua sehemu ya
kutua na kupaa ndege ya uwanja wa Tabora leo Januari 10, 2013 mara baada
ya kuzindua rasmi ujenzi wake
Waziri
wa Ujenzi Dkt John Pombe Magufuli (kulia) na Waziri wa Uchukuzi Dkt
Harrison Mwakyembe wakiongea wakati wa sherehe za uzinduzi wa ujenzi wa
uwanja wa ndege wa Tabora leo Januari 10, 2013
Rais
Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na balozi wa Tanzania nchini Afrika
Kusini Mhe Radhia Msuya mara baada ya kutua katika uwanja wa ndege wa
Kimataikfa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam akitokea mkoani Tabora
alikokuwa katika ziara ya kikazi ya siku tano kukagua shughuli za
maendeleo na kuzindua miradi mbalimbali.(PICHA NA IKULU)
,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,
SERIKALI imetangaza hatua kubwa na
kabambe za kufufua usafiri wa abiria na mizigo, ikiwa ni pamoja na
ununuzi wa mabehewa na injini za treni, katika hatua kubwa za aina yake
kuchukuliwa na Serikali kwa muda mrefu katika kurekebisha usafiri wa
treni nchini.
Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa
Harrison George Mwakyembe ametangaza hatua hizo leo, Alhamisi, Januari
10, 2013, wakati alipokuwa anamkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kuweka jiwe la msingi kwenye
ukarabati mkubwa wa Uwanja wa Ndege wa Tabora ikiwa ni tukio la mwisho
la ziara yenye mafanikio makubwa ya siku tano ya Rais Kikwete katika
Mkoa wa Tabora.
Mheshimiwa Mwakyembe amemwambia
Rais Kikwete na mamia kwa mamia ya wananchi waliohudhuria sherehe ya
uwekaji jiwe hilo la msingi kwenye Uwanja huo kuwa Wizara yake imeanza
kubadilisha reli nyepesi, iliyochakaa na yenye uzito mdogo kwa Reli ya
Kati.
Amesema kuwa kwa kupitia mashirika
yake ya RAHCO na Shirika la Reli Tanzania (TRL) Serikali itafanya
marekebisho hayo makubwa njia mzima ya Reli ya kati na kuwa mafundi wa
mashirika hayo tayari wamefika Mkoa wa Morogoro.
Waziri Mwakyembe amemwambia Rais
Kikwete kuwa Serikali kupitia Wizara yake na mashirika yake hayo,
imeagiza mabehewa mapya ya mizigo 274, imeagiza mabehewa mapya ya abiria
22, imeagiza mabehewa mapya ya kubebea kokoto 25 na pia imeagiza
mabehewa ya breki (brake vans) 34 na tayari malipo ya awali yamefanyika.
Katika namna inayothibitisha
dhamira ya Serikali kurekebisha hali ya usafiri wa reli nchini,
Mheshimiwa Mwakyembe pia amewaambia wananchi kuwa Wizara yake pia
imeagiza crane mpya na kubwa ya kubebea mizigo yenye uzito unaofikia
kilo 100.
Kuhusu injini za treni, Waziri Mwakyembe amemwambia Rais Kikwete kuwa zabuni kwa ajili ya kutengeneza upya (re-manufacturing) injini nane za treni imetolewa ili utengenezaji huo ufanyike, iwe ni ndani ama nje ya nchi.
Pia Waziri amesema kuwa oda
imetolewa kwa ajili ya utengenezaji wa injini mpya 13 za treni ambazo
malipo yake yatafanyika katika mwaka ujao wa fedha hata kama
utengenezaji wa injini hizo utaanza.
Aidha, Waziri amesema kuwa Wizara
kupitia mashirika yake hayo mawili imeagiza spea za kutosha kuweza
kufanya ukarabati mkubwa wa injini tano kwenye karakana zilizoko hapa
nchini.
“Mheshimiwa Rais, kwa hesabu
nyepesi tu ni kwamba katika kipindi kifupi tutaweza kuwa na injini kiasi
cha 26 ambazo zitarudisha uhai wa usafiri wetu wa reli kwa kiasi
kikubwa sana,” Waziri Mwakyembe amemwambia Rais Kikwete.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
10 Januari, 2013
No comments:
Post a Comment