|
Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo. |
GAZETI LA MTANZANIA DEC 26/ 2012.
JUKWAA
la Wakristo Tanzania (TCF) limeitaka Serikali na vyombo vya Usalama
kuchukua hatua za haraka kwa vikundi halifu vya kisiasa au kidini,
vinavyochochea uvunjifu wa amani na sheria nchini.
Jukwaa hilo, ambalo linajumuisha Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT),
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Makanisa ya
Kipentekoste Tanzania (PCT) na Kanisa la Waadventisti Wasabato (SDA).
Jukwaa
hilo, limesema tabia ya kuachia uchochezi wa kidini kuendelea, bila
hatua madhubuti kuchukuliwa ni udhaifu mkubwa unaoonyeshwa na Serikali.
Akizungumza
na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, wakati wa kutoa tamko
rasmi la Jukwaa hilo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT),
Askofu Peter Kitula, alisema umoja huo unasikitishwa na vitendo viovu,
ambavyo vimekuwa vikijitokeza kila kukicha.
Askofu Kitula ambaye
pia ni Askofu wa Kanisa la Afrika Inland Church Tanzania, katika
mkutano wa nne wa TCF, wajumbe walitafakari kwa undani juu ya kuzorota
kwa uhusiano wa dini mbili za Kikristo na Uislamu.
“Katika
mkutano wa nne wa Jukwaa la Wakristo Tanzania, tulitafakari kwa undani
kuzorota kwa uhusiano baina ya dini zetu za Kikristo na Kiislamu na
kutathmini wajibu wa kanisa na utume wake wa kinabii kwa taifa,” alisema
Askofu Kitula.
Alisema kutokana na muono wao, kwa kauli moja
walitaka lianzishwe baraza mahsusi ambalo litakuwa huru lisilo egemea
chama chochote cha kisiasa wala dini, likiwa na dhumuni kuu la kulinda
na kuiongoza Serikali.
“Baraza hili, litasaidia kuiongoza
Serikali dira na dhana ya utu katika mfumo wa uchumi wenye kujali
maslahi ya wote ambayo hayatapotoshwa, liwe na uwezo wa kuvichunguza
vyombo vya sheria na usalama, itakapotokea matatizo makubwa
yanayoashiria uvunjifu wa haki na kuteteresha usalama wa nchi,” alisema
Askofu Kitula.
Alisema viongozi wa dini zote za Kikristo,
Kiislamu, Kihindu na nyinginezo, wawafundishe waumini wao katika
mienendo mema, hasa vijana ili kuwajengea uelewa na utashi wa
kuvumiliana kwa upendo.
Alisema kuna masuala ambayo yanatakiwa kufafanuliwa na kudhibitiwa na dola mapema, ili yasiendelee kupotoshwa.
Alisema ni dhana potofu, kuwa Tanzania inaendeshwa kwa mfumo wa Kikristo.
Alisema
maneno hayo ni ushahidi wa uwepo wa ajenda za waumini wenye imani kali
na waliojiandaa kwa mapambano maovu kutetea dhana potofu na kinzani kwa
misingi ya demokrasia na haki za binadamu, kama ilivyotangazwa na Umoja
wa Mataifa.
“Pia ukiangalia kwa upande wa Zanzibar, asilimia 100
vingozi wa ngazi ya juu Serikalini ni Waislamu na sio kweli, Zanzibar
hakuna Wakristo wenye sifa za kuongoza, hata viongozi wa tume ya
mabadiliko ya Katiba, theluthi mbili ya wajumbe wake ni Waislamu.
“Watanzania
wanapaswa kuelewa kuwa nchi hii inaongozwa kwa misingi ya utawala wa
kisheria na si vinginevyo, hii ni mfano midogo tunayo mingine mingi
iliyowazi,” alisema Askofu Kitula.
Alisema katika mikataba ya
kumbukumbu, ‘memorandam of Understanding’ ya mwaka 1992, ambayo ilikuwa
kwa ajili ya huduma za kijamii ambazo zinaendeshwa na makanisa nchini
kote.
“Makubaliano hayo, yalilenga kutolewa kwa huduma za kijamii
zitolewe na makanisa kwa Watanzania wote, ikiwa pamoja na huduma za
hospitali, vituo vya afya, zahanati na shule mbalimbali zinazoendeshwa
na makanisa nchini kote.
“Ni vema Watanzania wakaelewa
makubaliano haya, yalikuwa kati ya makanisa ya Tanzania na makanisa ya
nchini Ujerumani, ambapo Serikali ya Tanzania ilihusishwa kwa vile raia
wake wangenufaishwa na misaada hii.
“Jukwaa la Wakristo Tanzania,
tunaitaka Serikali itoe tamko la ufafanuzi juu ya makubaliano hayo, ili
Watanzania waelewe maana, makusudi na manufaa kwa wananchi wote…
Kanisa
limeendelea kujishughulisha na huduma hizi kwa jamii hata kabla ya uhuru
na baada ya uhuru pasipo ubaguzi,” alisema Askofu Kidula.
GAZETI LA MWANANCHI. DEC 26/ 2012.
Maaskofu nchini watoa tamko zito.
Kwa ufupi
“Ukimya huu wa Serikali wakati kanisa linakashfiwa
unatoa taswira kwa viongozi wa makanisa kuwa Serikali inaunga mkono
chokochoko hizi…Kimsingi, unaponyamaza, maana yake unaunga mkono.”“Jambo
hili linavyoendelea kuachwa hivihivi inaashiria hatari kubwa ya
kiuhusiano siku za usoni, Tunaitaka Serikali ichukue jukumu lake la
msingi la kusimamia amani.”
MAASKOFU nchini, jana walitumia ibada za Krismasi kukemea maovu,
huku baadhi yao wakiwatuhumu matajiri nchini kuwa ndiyo kiini cha
vurugu zilizosababisha kuchomwa kwa makanisa yao hivi
karibuni.
Wakihubiri kwa nyakati na makanisa tofauti, viongozi hao
walisema uhasama huo dhidi ya Wakristo ulioanza kujengeka katika siku za
hivi karibuni, unafadhiliwa na baadhi ya matajiri kwa masilahi yao
binafsi.
Katika tamko lao lililotolewa na Umoja na
Makanisa Tanzania, maaskofu hao wameitaka Serikali kuchukua hatua dhidi
ya mbegu za chuki zinazopandikizwa ili kuwafarakanisha Watanzania kwa
misingi ya imani za dini.
Tamko hilo ambalo litarejewa Desemba 30, mwaka
huu, ni makubaliano ya pamoja kati ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT), Moravian, Anglikana, Pentekoste, Wasabato na Kanisa
Katoliki.
Askofu Dk Martin Shao wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini
akisoma tamko hilo wakati wa ibada ya pamoja, alidai kuwa baadhi ya
vyombo vya habari vya kidini, vinawachochea watu ili wawaue maaskofu na
wachungaji mbalimbali wa makanisa.
Pia, alihoji kauli zinazoenezwa kuwa nchi hivi
sasa inaongozwa kwa mfumo wa Kikristo ilihali asilimia 90 ya viongozi
wa juu nchini ni Waislamu.
“Labda niwakumbushe, viongozi wote waandamizi
wa ngazi za juu nchini, asilimia 90 ni Waislamu, itakuwaje nchi
iendeshwe kwa mfumo wa Kikristo?” alihoji Askofu Shao.
Aliwataja kuwa ni Rais na Amiri Jeshi Mkuu,
Makamu wa Rais, Mkuu wa Usalama wa Taifa, Jaji Mkuu na Inspekta Jenerali
wa Polisi (IGP).
“Kule Zanzibar, asilimia 100 ya viongozi wote ni
Waislamu na si kweli kwamba Zanzibar hakuna Wakristo wenye sifa ya
kuongoza,” alisema na kuongeza:
“Hata uwakilishi kwenye Tume kama ya kuandikwa
kwa Katiba Mpya, theluthi mbili ya wajumbe wake ni Waislamu…
Nchi hii
haina mfumo wa Kikristo, bali ni nchi yenye mfumo wa
kidemokrasia.”
Aliitaka Serikali ithibitishe ukweli kuwa haiendeshwi kwa
mfumo wa Kikristo badala ya kukaa kimya wakati maneno hayo ya uchochezi
yanaenezwa hadharani.
“Ni wakati wa kukubali kuwa misingi ya haki,
amani na upendo katika taifa letu imetikiswa kwa kiwango kikubwa.
Kumekuwapo na dalili za wazi za uchochezi na kashfa dhidi ya Ukristo,”
alidai.
Maaskofu hao wamewalaumu baadhi ya viongozi wa dini kutumia
vyombo vya habari vya kidini, vipeperushi, mihadhara na kanda za video
kukashfu dini nyingine.
“Ukimya huu wa Serikali wakati kanisa
linakashfiwa unatoa taswira kwa viongozi wa makanisa kuwa Serikali
inaunga mkono chokochoko hizi…Kimsingi, unaponyamaza, maana yake unaunga
mkono.
”“Jambo hili linavyoendelea kuachwa hivihivi inaashiria hatari
kubwa ya kiuhusiano siku za usoni.
Tunaitaka Serikali ichukue jukumu
lake la msingi la kusimamia amani.”
Askofu Pengo.
Katika
mahubiri yake jana, Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es
Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo aliwaponda matajiri
wanaojivunia mali, akisema siyo kigezo cha mtu kuwa na furaha maishani.
Kadinali Pengo alisema hayo katika misa ya
mkesha wa Krismasi iliyofanyika juzi katika Parokia mpya ya
Mongolandege, Ukonga, Dar es Salaam.
Alisema ni makosa mtu kuhesabu mali kama sehemu ya mafanikio katika maisha kwani kuna wenye mali nyingi ambao hawana furaha.
“Utajiri unaambatana na shaka, hofu na
wasiwasi kwa kufikiri kuwa huenda mali hii isinitoshe au itachukuliwa na
watu wengine,” alisema Kadinali Pengo na kuongeza.
“Tusitafute mali
kiasi cha kuwafanya watu wengine waumie, wahuzunike.
Kila mmoja atimize
wajibu wake pale alipo, matokeo yake ndiyo yatakayoleta furaha.”
Askofu Mhongolo.
Kwa upande wake, Askofu
wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kati, Godfrey Mhogolo amewataka
waumini kuendelea kuienzi Krismasi kwa kujali na kuwekeza katika elimu
ambayo ni msingi wa mambo yote.
Kiongozi huyo alisema kwa Wakristo, kuwa na
dhana ya kujenga elimu katika maisha yao itawasaidia kujiletea heshima
na kwamba watakuwa juu.
Askofu huyo alisema dhana nzuri ya kuthamini
elimu hadi sasa waumini wa Kikristo nchini wamekuwa ni mfano wa kuigwa
na jamii na taifa kwani kati ya jumla ya vyuo vikuu 19 vilivyoko nchini
vyuo saba vinamilikiwa na Wakristo, 11 na Serikali huku kimoja kikiwa
cha Kiislamu.
Askofu Mkude.
Askofu Thelesphory Mkude wa Jimbo
la Morogoro amewataka waumini wa dini zote kushiriki vyema katika
kuendeleza na kushika neno la Mungu na kuombea nchi hasa katika kipindi
hiki cha kufunga mwaka na kukaribisha Mwaka Mpya.
Katika ibada ya
mkesha wa Krismasi, Askofu Mkude alisema kuwa imefikia wakati sasa wa
kumshirikisha Mungu kila jambo kwani kila siku matendo maovu yanaendelea
kutokea na kusababisha kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.
Askofu Sehaba.
Askofu
wa Kanisa Kuu la Anglikana, Dayosisi ya Morogoro, Godfrey Sehaba
ameitaka Serikali kuchukua hatua za haraka pale inapoona kuna tishio la
uvunjivu wa amani nchini kuliko kukaa kimya na kusubiri likitokea ndipo
ianze taratibu za kudhibiti.
Alisema kumekuwapo na vitendo vya
uvunjifu wa amani vinavyofanywa na baadhi ya waumini wa dini kama
uchomaji wa makanisa na kusema Serikali inapaswa kutovifumbia macho.
Askofu Mwombeki.
Askofu Edson Mwombeki wa Kanisa la Free Evangelism Tanzania amewataka Watanzania wote kulinda amani na utulivu.
Akihubiri
kwenye ibada ya Krismasi iliyofanyika katika Manispaa ya Shinyanga,
aliwaomba Watanzania wote wabadilike na kuwa na tabia njema kwani kwa
sasa watu wengi wamepoteza uadilifu, amani na uzalendo.