DAR ES SALAAM, Tanzania
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amepiga
marufuku na kuagiza kuondolewa vizuizi vyote vilivyoanzishwa na Halmashauri
kwenye stendi za barabara kubwa kwa ajili ya kukusanya ushuru kwani vinaleta
usumbufu kwa abiria.
Kauli hiyo ilitolewa waziri huyo jijini Dar es
Salaam, wakati alipofanya ya ziara ya kushtukiza kwenye Kituo cha Mabasi
yaendayo mikoani na nje ya nchi majira ya saa 11:30 alfajiri, ili kujionea utendaji kazi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri
wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), na Kikosi cha Usalama
Barabarni (Trafic), haswa katika udhibiti wa nauli holela katika kipindi hiki
cha sikukuu ya Chrismas na mwaka mpya.
Alisema uwamuzi wake huo unatokana na kubaini kuwa
Halmashauri hizo, zimekuwa zikiwalazimisha madereva kuingiza magari (Mabasi),
kwenye vituo hivyo ambavyo siyo rasmi
kwa lengo la kujikusanyia ushuru.
Amevitaja vituo hivyo vilivyolalamikiwa kwa
usumbufu huo, kuwa ni pamoja na Mafinga, Kibaigwa, Nzega, Kibaha na vingine.
“Madereva wamekuwa wakilazimishwa kuingia katika
stendi hizi hata kama hawana abiria wakushuka amakupakia, kitendo ambacho
kinawapotezea abiria muda wao wakufika kule wanakokwenda bila sababu za
msingi”alisema Dk Mwakyembe.
Alisema utaratibu huo haukubaliki, endapo ukiachwa
uendelee hivyo iko siku watazuka watu watafikia hatua ya kuanzisha vizuizi kama
hivyo majumbani mwao lengo likiwa ni kuibia wananchi.
Dk Mwakyembe amezitaka Halmashauri hizo kuacha
utaratibu huo na baadala yake watafute vyanzo vingine vya ukusanyaji mapato.
Katika hatua nyingine Dk Mwakyembe amewaonya baadhi
polisi wa kikosi cha usalama barabarani kutokana na mtindo wao wakusimamisha
magari kwa kushtukiza wakitokea vichakani.
Alisema malalamiko hayo ameyesikia siku nyingi
hivyo ameahidi kuwa atayafanyia kazi, ambapo aliwatahadharisha askari wenye
tabia kama hizo, watambuwe muda wao sasa unahesabika.
Akizungumzia hali ya usafiri katika kipindi hiki
cha sikukuu hizo mbili, Alisema hali aliyoikuta Kituoni hapo inaridhisha
kwakuwa abiria wote kwenye mabasi walikuwa wamepata tiketi kwa bei elekezi ya
Sumatra.
Dk. Mwakyembe alitoa wito kwa abiria wote kuwa
wahakikishe wanatoa ushirikiano kwenye vyombo vinavyohusika pindi watakapotozwa
nauli kinyume na ile ya kawaida.
“Msikubali kulipishwa zaidi toeni taarifa haraka,
hata katika nauli za mizigo msikubali kulipia mzigo wa kilo 20 atakaekubali
yote hayo mtambue amejitakia mwenyewe na asilaumiwe mtu”alisema.
Naye Kaimu Mkurugezi Udhibiti Usafiri wa Barabarani
(Sumatra), Leo Ngowi, alisema katika operesheni inayoendelea ya kuyakamata
magari yanapandisha nauli holela jana, walifanikiwa kulikamata basi la Kampuni
ya KVC lenye usajili namba T709AAT.
Alisema gari hilo lilikwenda kinyume kwa kuwatoza
nauli ya sh 35,000 baadala y ash 25,000 abiria waliokuwa wakisafiri kwenda
Arusha.
Aidha, Sumatra imetoa leseni za muda kwa wamiliki
magagri ambayo yamekidhi viwango vilivyohitajika na mamlaka hiyo, yenye uwezo
wa kuchukua abiria 30 kwa lengo la kusaidia kusafirisha abiria wanaofika kwa
wingi kituoni hapo ambapo mikoa inayoongoza kwa abiria ni Kilimanjoro, Arusha
na Mwanza.
No comments:
Post a Comment