Wednesday, August 22, 2012

MAHAKAMA KUU NZEGA




M
ahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, imetengua matokeo ya uchaguzi mdogo katika jimbo la Igunga mkoani Tabora, baada ya kubainika kuwa uchaguzi huo ulitawaliwa na vitendo vya rushwa, kampeni chafu na vitisho dhidi ya wapiga kura.
Jaji Mary Nsimbo Shangali wa mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, alitangaza kutengua matokeo hayo baada ya mahakama hiyo kuridhika na hoja saba  zilizowasilishwa na upande wa mlalamikaji  kati ya hoja  17 zilizowasilishwa katika mahakama hiyo.
Kesi hiyo ilifunguliwa na Mlalamikaji aliyekuwa mgombea wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)  Joseph kashindye, ambaye aliwakilishwa na wakili Maarufu nchini Profesa Abdallah Safari  ambapo alipinga mtokeo ya uchaguzi huo akilalamikia kukiukwa kwa sheria ya uchaguzi mkuu.
Upande wa Utetezi  uliwakilishwa na  mawakili Mohamed Salum Malik na Gabriel Malata kutoka ofisi ya Mwanasheria mkuu wa serikali, Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Igunga,  na mawakili Antony Kanyama na Kamaliza Kayaga waliokuwa wakimtetea mbunge wa Igunga Peter Dalali Kafumu.
Akisoma hukumu hiyo iliyochukua saa nne, Jaji Shangali alisema kuwa mahakama imeridhika na upande wa mlalamikaji katika malalamiko yake saba, ambayo alisema yanathibitika na kuonyesha kuwa uchaguzi huo mdogo wa jimbo la Igunga haukuwa huru na haki.
Alivitaja baadhi ya kasoro zilizopelekea kutengeliwa kwa uchaguzi huo ni pamoja na  Ahadi  iliyotolewa na Waziri wa Ujenzi  Dk. John Pombe Magufuli, kuhusu  ujenzi wa daraja la Mbutu ambalo alidai kwamba  kama wananchi hawataichagua CCM daraja hilo halitajengwa, wakati ambapo katika kipindi hicho kulikuwa na shida kubwa ya usafiri katika eneo hilo.
Alisema Pia Waziri huyo alitumia nguvu  na kuwatisha wapiga kura kwamba kama hawatamchagua mgombe wa chama cha mapinduzi katika Uchaguzi huo watawekwa ndani kitu ambacho alisema kinatishia uchaguzi huo kuwa huru na wa haki.
Alisema Kitendo pia kilichofanywa na mbunge wa Tabora mjini Ismail Aden Rage, hakikuwa cha uungwana kwani alitumia lugha ya uongo kwa lengo la kupotosha wapiga kura ambapo alidai mgombea wa chama cha Demokrasia na Maendeleo  ( Chadema) amejitoa katika uchaguzi huo.
Alisema pia mbunge huyo alihusika katika vitendo vya kujenga hofu kwa wapiga kura baada ya kupanda jukwaani na Bastola, hali ambayo iliwafanya wapiga kura kuhofia na hivyo kuleta dosari katika uchaguzi huo hoja ambayo alisema imezingatiwa na mahakama.
Jaji huyo wa Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Tabora,  alioonyesha kusikitishwa na kitendo kilichofanywa na imamu wa Msikiti wa Ijumaa wa Igunga, Sheikh Swaleh Mohamed, kutangaza msikitini kwa waumini wa dini ya kiislamu wasikichague chama cha Chadema kwa sababu viongozi wake wamehusika kumdhalilisha aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Igunga, Fatma Kimario.
Jaji Mary pia aliithibitisha kauli iliyotolewa na katibu mkuu wa chama cha mapinduzi Wilson Mkama,  kuwa chama cha Chadema kimeingiza makomandoo katika wilaya ya Igunga kwa lengo la kuvuruga uchaguzi huo mdogo ilikuwa na madhumuni ya kupeleka vitisho kwa wananchi.
Jaji Mary pia alisema kitendo cha serikali kugawa mahindi ya msaada kwa wakazi wa Igunga katika kipindi cha kampeni kitu ambacho kimeleta fadhaa kubwa kwa wapiga kura, huku akihoji je ni nani aliyekufa njaa katika kipindi hicho na kwamba kulikuwa na umuhimu gani wa kugawa mahindi katika kipindi cha kampeni.
Kuhusu hoja iliyotolewa na upande wa utetezi  ya kumtaka mlalamikaji kuwasilisha malalamiko yake kwa tume ya Taifa ya Uchaguzi badala ya kuyafikisha mahakamani, alisema kuwa hoja hiyo haina mashiko na kwamba mlalamikaji anahaki ya kupeleka malalamiko hayo katika mahakama kuu.
Kutokana na kasoro hizo, Jaji Mary alitangaza rasmi kutengua matokeo ya uchaguzi mdogo wa jimbo la Igunga na kuigaza tume ya Taifa ya uchaguzi kufuata taratibu za kufanya mchakato mwingine wa uchaguzi katika jimbo hilo.
Aliuagiza upande wa walalamikiwa ambao ni msimamizi wa Uchaguzi, Mwanasheria mkuu wa serikali na aliyekuwa mbunge wa Igunga, Peter Dalali Kafumu kulipa gharama zote za kesi hiyo.
Mamia ya watu walijitokeza kusikiliza hukumu huyo na mara baada ya kutolewa mamia ya wafuasi wa Chadema walikuwa wakishangia kwa nguvu, shamrashamra, vifijo na kisha kufanya maandamano yasiyokuwa rasmi kwa dakika kadhaa huku mashabiki, wanachama na wapenzi wa chama cha mapinduzi wakionekana kuduwaa na kutoamini kilichotokea katika mahakama.
Mahakama kuu ya Tanzania ilianza kusikiliza kesi hiyo Machi 26 mwaka huu, baada ya mgombea huyo wa Chadema kufungua malalamiko yake novemba mwaka jana, baada ya uchaguzi huo mdogo kufanyika oktoba 2 mwaka jana, kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa mbunge wa Jimbo hilo kwa miaka 14 Rostam Aziz.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment