Friday, January 11, 2013

POLISI TABORA WAKOSANYA ZAIDI YA MILIONI 400

Na Lucas Raphael,Tabora

Jeshi la Polisi mkoani Tabora, limesema kuwa  limekusanya kiasi cha shilingi milioni 445.9 kwa kipindi cha mwaka jana, ikiwa ni fedha zilizotokana na tozo za  adhabu za makosa ya usalama barabarani.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Tabora, ACP Antony Ruta, amesema kuwa kiasi hicho cha fedha zilizokusanywa na jeshi hilo kimetokana na makosa  14,604 yaliyofanyika katika kipindi cha mwaka jana katika wilaya zote saba za mkoa huo.

Alisema kwa mujibu wa takwimu hizo idadi ya makosa ya usalama barabarani yaliyofanywa na madereva katika mkoa huo imeoongezeka kwa aslimia 100 ikilinganishwa na makosa ya usalama barabarani yaliyofanywa  mwaka juzi ambayo ni 7,589 na kuingiza shilingi milioni 196.5 kutokana na tozo za makosa hayo.

Akizungumzia takwimu za makosa ya jinai yaliyofanyika katika mkoa huo kwa kipindi cha mwaka jana, Kamanda Ruta, alisema kuwa jumla ya makosa 18,586 yamefanyika katika mkoa huo na kulipotiwa katika vituo mbali mbali vya polisi ikilinganishwa na makosa 19,172 yaliyofanyika kwa kipindi cha mwaka juzi. Kukiwa na upungufu wa makosa 586.

Akizungumzia takwimu zilizotokana na vifo vilivyosababishwa na ajali za barabarani,  kamanda alisema kuwa jumla ya watu 152 walipoteza maisha katika matukio  118 ya ajali yaliyotokea mkoani Tabora kwa kipindi cha mwaka jana huku watu 765 wakijeruhiwa na baadhi yao wakipata ulemavu wa kudumu.

Kamanda alitoa wito kwa madereva kuendesha magari kwa tahadhari kubwa, kuepukana na mwendo kasi usiokuwa wa lazima na kufuata sheria na taratibu ili kuokoa maisha ya abiria wasiokuwa na hatia.


Mwisho.

No comments:

Post a Comment