Tuesday, January 1, 2013

"KUKATAA KUWEPO TEN PERCENT KWENYE MIRADI KWANIPONZA"

Na Hastin Liumba,Uyui
 


 
 
SAKATA la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Uyui, kumvua cheo cha ukuu wa idara ya maji, injinia Nestory Nicodemus, kwa tuhuma kadhaa, limechukua sura mpya baada ya injinia huyo kudai anawasiliana na wanasheria wake ili haki itendeke.
 
Akizungumza na waandishi wa habari, injini Nestory Nicodemus, alisema kuwa suala lake limeendeshwa kimajungu na  uonevu na kwamba ametolewa kafara kwa chuki za baadhi ya watu.
 
Nicodemus alisema awali aliundiwa tume ya uchunguzi ambayo haikuzingatia kuwepo kwa changamoto kadhaa katika kile kinachoelezwa kuwa anatuhumiwa kwa uzembe, katika upotevu wa vifaa vya gari, kutokamilika kwa mradi wa maji na ujenzi wa vyoo 6 katika kata ya Kizengi.
 
“Tume niliyoundwa iliegemea upande mmoja na kwamba katika uchunguzi wao hawakuzingatia changamoto zilizoko kwenye miradi ninayotuhumiwa kutoikamilisha kwa wakati…..hii ni uonevu kwangu ikiwa ni kwa maslahi ya wachache wanaopenda ten percent.” Alisema
 
Akifafanua juu ya tuhuma hizo, injinia huyo alisema kuwa kuhusiana na mradi wa Water Sector Development Project-WSDP ulipatiwa kiasi cha sh milioni 20 ili kutekeleza ujenzi wa vyoo 6 lakini baadhi ya vifaa vilitumika kujenga nyumba kadhaa za walimu wa kata ya Kizengi.
 
Alisema licha ya mradi huo kutokamilika kwa wakati, tayari vyoo vitatu vilishakamilika, huku choo kimoja kikijengwa na wananchi, hali hiyo ya ujenzi wa nyumba za walimu na kutumika vifaa kadhaa kwenye ujenzi wa nyumba za walimu ndizo sababu zilizopelekea kutokamilika mradi huo kwa wakati na taarifa zake zipo.
 
Kuhusu tuhuma za kushindwa kukamilika kwa mradi wa maji makao makuu ya wilaya ya Uyui, Isikizya, alisema zipo sababu za msingi kwa mkandarasi aliyepewa kazi hiyo, PET Company Ltd, alipewa miezi mitano katika kazi yake ya uchimbaji wa mtaro lakini kutokana na mtaro huo kupita eneo la mashamba ya tumbaku wananchi waliomba hadi mavuno yao yaishe na mradi huo haukuwa na fedha za fidia.
 
Aliongeza kuwa suala hilo ofisi ya mkurugenzi ilikuwa na taarifa ikiwemo taarifa za mkandarasi kuomba siku 90 zaidi ili kukamilisha mradi huo, huku mradi huo pia ukichelewa kutokana na eneo hilo pia kuwa na mwamba na hivyo kazi hiyo kuwa ngumu na ya muda mrefu.
 
Kuhusu tuhuma za kutakiwa kurejesha kiasi cha sh milioni 4,420,640 ndani ya siku saba, ambazo zingejenga vyoo sita vya kata ya Msimba na Kizenge, inamshangaza kwani fedha hizo zipo kwenye akaunti benki kwani kama fedha hazikutumika ina maana zipo na hakuna wizi.
 
Alisema tuhuma nyingine ni kuhusiana na ununuzi wa mashine ya maji ya Diesel badala ya umeme, injinia Nicodemus alisema alifanya hivyo kutokana na agizo la aliyekuwa waziri wa maji Profesa Mark Mwandosya, kipindi cha mwaka 2010 alipofanya ziara kwani hakuwa na jinsi kutengua agizo la waziri hasa kutokana na kipindi hicho makao makuu ya wilaya hayakuwa na umeme.
 
Alisema maamuzi ya ununuzi wa mashine hiyo pia yalipitia kwenye vikao vya zabuni na taarifa zake zipo, huku suala la upotevu wa vifaa katika stoo ya maji kama mkuu wa idara liliripotiwa kituo cha polisi na uchunguzi unaendelea huku kampuni ya ulinzi ikijulishwa suala la mtumishi wao kuhusika na upotevu wa vifaa hivyo.
 
Aliongeza kuwa alichukua hatua kama mkuu wa idara ambaye anamwakilisha mwajiri wake ambaye ni mkurugenzi.
 
Alimalizia kuwa kutokana na maamuzi ya madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Uyui kuketi kwenye kikao cha baraza maalumu na kumvua madaraka, amewasiliana na wanasheria wake kuangalia hatua za kuchukua ili haki zake kama mwajiriwa zipatikane.
 
Mnamo mwezi desemba 19 mwaka 2012 baraza la madiwani maalumu liliketi na kuazimia kumvua madaraka injini Nestory Nicodemus kwa uzembe wa tuhuma ainishwa.

No comments:

Post a Comment