TAARIFA
YA MHE. JANUARY Y. MAKAMBA (MB), NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO, SAYANSI
NA TEKNOLOJIA KUHUSU USITISHAJI WA MATANGAZO YA ANALOJIA NA KWENDA
KATIKA MFUMO WA DIJITALI
Ndugu Wananchi,
Mtakumbuka
kuwa hapo tarehe 23 Februari 2012 tuliwatangazia kupitia vyombo vya
habari juu ya usitishwaji wa matangazo ya televisheni kwa kutumia
teknolojia ya analojia kwenda katika mfumo mpya unaotumia teknolojia ya
dijitali.
Napenda
kuwaleleza kuwa, maandalizi ya kuzima mitambo ya analojia kuanzia
tarehe 31 Desemba 2012 yamekamilika kwa mujibu wa makubaliano ya nchi
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hata hivyo, napenda sasa kutoa taarifa kuwa uzimaji wa mitambo ya analojia utafanyika kwa awamu kama ifuatavyo:-
(1) Dar Es Salaam-31 Desemba, 2012;
(2) Dodoma & Tanga- 31 Januari, 2013;
(3) Mwanza-28 Februari, 2013;
(4) Moshi & Arusha-31 Machi, 2013;
(5) Mbeya-30 Aprili, 2013.
Tumeamua kuanza kuzima mitambo hiyo kwa Jiji la Dar es Salaam kwanza ili
kutoa fursa kwa makampuni yenye leseni kusimika mitambo ya utangazaji
wa dijitali katika mikoa mingine. Makampuni haya yamejipanga kukamilisha
usimikaji wa mitambo hiyo katika mikoa minane katika miezi minane
ijayo.
Mitambo
ya analojia itakayozimwa kesho ni ile iliyopo Kisarawe na Makongo.
Vituo ambavyo siku ya tarehe 1 Januari 2013, vitapaswa kuanza kutangaza
matangazo kwa mfumo wa dijitali ni TBC1, ITV, EATV, Channel 10, StarTV,
DTV, CapitalTV, TumainiTV, ATN, MlimaniTV, C2C, CTN, CloudsTV na Efatha.
Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inafanya jitihada za kutosha kuhakikisha
kwamba makampuni yenye leseni za kusambaza ving’amuzi yanakuwa na
ving’amuzi vya kutosha na vingine vimeagizwa ili kukidhi mahitaji ya
baadaye na vile vilivyopo sokoni vina ubora unaokubalika.
Vilevile,
Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
itahakikisha kwamba zoezi la uhamaji linafanyika bila usumbufu na kero
kwa wananchi. Makampuni yanayouza ving’amuzi yameagizwa yaimarishe
huduma kwa wateja wakati wa kuuza ving’amuzi na hata baada ya ununuzi
iwapo wananchi watakuwa na matatizo na ving’amuzi.
Zoezi
hili la uhamaji ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu. Tutakapokuwa
tumekamilisha uhamaji, huduma za mawasiliano na utangazaji zitapanuka
na kuwa bora zaidi. Kwa mfano, itawezekana sasa kuangalia televisheni
kupitia simu zetu za mikononi. Vilevile, itawezekana, kwa bei nafuu
kabisa, kwa mtu mwenye uwezo wa kutengeneza vipindi kukodisha chaneli
yake na kutangaza vipindi vyake. Vilevile, bei za mawasiliano na
utangazaji zitashuka, na tutakuwa tumepiga hatua kubwa kwenye mapinduzi
ya teknolojia duniani, ambayo nchi yetu haiwezi kubaki nyuma.
Ndugu Wananchi,
Serikali
kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania itaendelea kutoa
elimu kwa wananchi kuhusu uhamaji huu. Serikali inatarajia kupata
ushirikiano wa karibu kutoka kwa wadau wa sekta ya utangazaji na
wananchi kwa ujumla katika kipindi cha uzimaji wa mitambo ya utangazaji
wa televisheni ili kufanikisha zoezi la uzimaji wa mitambo ya utangazaji
ya teknolojia ya analojia.
Uhamaji
huu hautahusu televisheni za wananchi zinazopata matangazo kupitia
madishi (nyungo) (satellite) au nyaya (cables). Hivyo, wananchi
wanaopata matangazo kupitia DStv, Zuku, na nyinginezo wataendelea kupata
matangazo yao kama kawaida.
Ndugu Wananchi
Kama
kuna mwananchi yoyote ana kero, malalamiko, swali au anahitaji
maelekezo kuhusu uhamaji, awasiliane na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA) kupitia namba 0784-558270; 0784558271 au barua pepe:
malalamiko@tcra.go.tz
Ndugu Wananchi,
No comments:
Post a Comment