uFISADI - Tabora
Baraza la madiwani la
halmashauri ya manispaa ya Tabora, limekataa kupokea taarifa ya utekelezaji wa
miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo baada ya taarifa hizo kuwa na
kasoro na kuonyesha uwepo wa vitendo vya ubadhilifu na kifisadi.
Baraza hilo lililokutana katika
kikao maalum kwa ajili ya kujadili hoja maalum ya kupokea taarifa hizo za
miradi ya maendeleo lilikuwa kali na mara kadhaa madiwani walimpa onyo na
tahadhari mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuwa makini na Wataalam wake.
Akitoa hoja kuhusu kasoro za
taarifa hizo, Diwani wa Kata ya Mbugani, Idd Kapama, alisema kwamba
kumekuwa na taarifa za mashaka kuhusu ujenzi wa barabara za manispaa ya
Tabora ambapo kiwango cha fedha kilichotolewa ni kidogo ikilinganishwa na
makisio.
Hata hivyo alisema kuwa katika
taarifa moja inaoonyesha kuwa ujenzi wa barabara hiyo umekamilika lakini
utekelezwaji wake ni asilimia 30, huku vifusi vikiwa bado havijasambazwa lakini
mkandarasi amelipwa malipo yote ya gharama za ujenzi ambazo shilingi milioni
150.
Kuhusu udhaifu wa halmashauri
ya manispaa ya Tabora kutokuwa imara katika usimamizi na ukusanyaji wa
mapato Diwani wa Kata ya Ndevelwa, Selemani Maganga alisema kuwa
inasikitisha kuiona halmashauri kubwa kama hii ikiwa haina fedha.
Kisha akalalamikia kitendo cha
Halmashauri ya Manispaa kuendelea kudaiwa na watumishi ama wazabuni na madeni
husika kuongezeka na kufikia viwango vikubwa bila ya kuwepo kwa sababu za
kueleweka hali ambayo imeifanya halmashauri kudhoofika.
Mkurugenzi wa manispaa ya
Tabora, Mariam Makandawa, alisema kuwa hali ya kifedha katika halmashauri
si nzuri na kwamba halmashauri imekuwa ikiweka mikakati itakayohakikisha kwamba
wadai wa halmashauri hiyo wanalipwa ikiwa ni pamoja na kuongea nao ili kupata
maridhiano.
Hata hivyo kikao hicho
kilikataa kupokea taarifa zote zilizowasilishwa na kuamua kwa kauli moja
kumuomba mkuu wa mkoa wa Tabora, Fatma Mwassa, aunde tume kwa ajili ya
kuchunguza vitendo vya ubadhilifu na ufisadi vinavyofanywa na baadhi ya
watumishi na wakuu wa idara katika halmashauri ya manispaa ya Tabora.
Hii ni mara ya kwanza kwa Baraza la madiwani
la Halmashauri ya manispaa hiyo kutoa maamuzi ya kumtaka mkuu wa mkoa aunde
tume kwa ajili ya kuchunguza ubadhilifu na vitendo vya kifisadi toka
halmashauri hiyo ilipoanzishwa mwaka 1984.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment