DR. STEVEN ULIMBOKA KATIKA PICHA TOFAUTI.
JESHI la Polisi nchini limesema linamsubiri Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka kufika polisi na kutoa
taarifa yake rasmi kuhusu tukio lililomtokea Juni 26, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Mwananchi , msemaji wa jeshi la Polisi Advera
Senso amesema wanamsubiri Dk Ulimboka afike polisi na kutoa taarifa yake rasmi
pamoja na ushirikiano ili wapate kujua nini kilichotokea.
“Wakati ule hatukumhoji kwa kuwa alikuwa anaumwa tokea hapo,
hatujapata taarifa yake hivyo, sisi tunamsubiri aje kutoa taarifa yake na atupe
ushirikiano katika suala hilo, tunataka kujua hali yake, lakini sisi
tunamsubiri aje ili tupate ushirikiano wake.”
Kabla ya polisi kutoa taarifa hiyo, Oktoba 28, mwaka huu, Dk
Ulimboka aliibuka na kusema yuko imara na anajiaanda kuanika waliomteka,
kumtesa na kisha kumtupa katika Msitu wa Mabwepande, nje kidogo ya Jiji la Dar
es Salaam.
Dk Ulimboka alisema kuwa kamwe hajanunuliwa na kuwa kwake
kimya kwa muda mrefu kumetokana na kufuatilia kwa karibu masharti ya matibabu
yake na si vinginevyo.
“Sijanunuliwa, sijawaogopa watesi wangu, wala
sijanyamazishwa kwa lolote lile. Hata hao wanaoeneza taarifa kuwa nimenunuliwa,
wanajua kuwa hawana ubavu wa kuninunua.
Bali kimya changu kimetokana na kufuata
masharti ya daktari wangu,” ameeleza Dk Ulimboka kujibu swali iwapo kimya chake
kimetokana na kununuliwa.
Dk Ulimboka alikiri kuwa amewahi kusikia taarifa za yeye
kununuliwa na kwamba huwa anajisikia vibaya anapoona kuna kundi la watu
linahaha kutaka kupotosha ukweli na kuchafua jina lake.
“Huo ni uzushi mtupu.
Hata walionitesa wanajua kuwa hawawezi
kuninyamazisha au kuninunua.
Wanajua sina bei katika kutetea masilahi ya Umma.
Ndiyo maana wakaamua kutumia njia ile ya kinyama kutaka kunitoa roho yangu.
Siwaogopi wanaodhuru mwili bali yule awezaye kutoa roho.
Nakuhakikishia, muda
si mrefu nitaanika kila kitu juu ya kutekwa kwangu, kuteswa na kutupwa kwenye
msitu wa Mabwepande,” ameeleza.
Juni 26, 2012, Dk Ulimboka alitekwa na kuteswa vibaya ambapo
alinyofolewa kucha na kutolewa meno na hatimaye kutupwa katika msitu wa
Mabwepande.
Mwenyekiti huyo wa Jumuia ya Madaktari Tanzania , aliokolewa
asubuhi yake na wasamaria wema karibu na msitu huo, Bunju nje kidogo ya Dar es
Salaam.
Akizungumza kwa sauti ya kujiamini, Dk Ulimboka, ambaye bado
hajahojiwa na polisi wa Tanzania juu ya aliowataja, amesisitiza kuwa
alipokamatwa alikuwa na akili timamu na kwamba waliopanga mkakati wa kumteka
anawafahamu.
No comments:
Post a Comment