Friday, December 7, 2012

MWANAHARAKATI WA HAKI ZA BINADAMU AUAWA MKOANI MARA TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KIFO

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KIFO CHA MTETEZI WA HAKI ZA BINADAMU
 
Mitandao ya Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania na ule wa Watetezi Mashariki na Pembe ya
Afrika (EHAHRDN) imepokea kwa mshituko mkubwa kifo cha mtetezi wa haki za binadamu
Eustace Nyarugenda.
 
Mshituko huo unatolewa katika tamko la pamoja lililoandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za
Bindamu Tanzania (THRD), Shirika la Kivulini lenye makao yake jijini Mwanza, na shirika
alilokwa akilifanyia kazi marehemu la ABC-Foudation. Mashirika mengine wanachama kutoka
Kanda ya Ziwa na nchi nzima pamoja na watu binafsi pia wameonyesha kuguswa na msiba huo ni
kusema ni pigo kubwa kwa watetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania na katika ukanda wote
huo wa Ziwa.
 
Tayari Jeshi la Polisi kupitia kwa Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Mara Japhet Lusingu – SSP
aliyesema katika taarifa yake kwa wanahabari kwamba marehemu alifariki dunia kabla ya kupatiwa
matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Bunda alipofikishwa kwa ajili ya kujaribu kuokoa maisha
yake.

Tarifa hiyo ya polisi ilisema kwamba marehemu alikutwa katika nyumba ya kulala wageni
iitwayo Savana Bar and Guest House katika chumba namba 4 akiwa anakoroma baada ya kuvunja
mlango wa chumba hicho alichokuwa amepanga siku hiyo ya tukio majira ya saa 12.30 jioni.
 
Marehemu alikutwa akitokwa na mapovu mdomoni huku mezani kukiwa na chupa ya bia aina ya
Castle Milk iliyotumika ikiwa na pombe kidogo na chupa ya dawa ya kuulia wadudu aina ya Nivan.
Nyarugenda ambaye pia alikuwa mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na
Watoto la Action Based Community Foundation ambalo ni mwanachama, alipotea siku ya Jumatatu
tarehe 03 ya mwezi huu majira ya saa 12:00 asubuhi. Aliondoka nyumbani kwake akiwa amevaa
kaptula ya jeans rangi ya blue, tisheti na kandambili na mkononi akiwa amebeba kitabu cha kumbu
kumbu.
 
Kwa mujibu wa msaidizi wake Bw. Andreas Migiro, aliyepo katika semina ya watetezi wa haki za
binadamu jijini Dar es Salaam na binti wa marehemu anayeitwa Wema, hii ni mara ya pili kwa
marehemu huyo kupotea katika mazingira yenye utata. Tukio la kwanza lilitokea mwezi Agosti
mwaka jana na marehemu alipatikana baada ya siku nne akiwa katika hali dhaifu. Tukio la pili
limekuja baada ya mtetezi huyo kumuaga binti yake kwamba atakuwepo mjini Musoma kwa muda
na kisha ataelekea mjini Tarime.

Kwa mujibu wa Migiro katika tukio la awali wadau mbali mbali likiwamo shirika la Kivulini lilipo
jijini Mwanza walitoa ushirikiano mkubwa hadi kupatikana kwa mtetezi huyo mjini Bariadi.
Uchunguzi wa kitabibu kutoka Hospitali ya Rufaa ya Bugando ya jijini Mwanza, ulionyesha
kwamba hapakuwapo na ushahidi wa kuwekewa sumu au kitu chenye madhara kwa mtetezi huyo
mara alivyopotea mara ya kwanza. 

Hata hivyo baada ya kurejea ofisini alionyesha kuwa mwenye
dalili za kuathirika kisaikolojia lakini baadaye hali hiyo ilipotea na akaendelea na kazi kama
kawaida hadi lilipotokea tukio hili la kifo.
 
Mara ya mwisho mtetezi huyo alikuwa anaendesha zoezi la kongamano la siku 16 za kupinga
unyanyasaji wa kijinsia lililofadhiliwa na shirika la kutetea haki za wanawake na watoto la
WILDAF. 

Kupotea kwake na hatimaye kifo chake huenda kukahusishwa na shughuli zake za
kupinga vitendo viovu dhidi ya wanawake na watoto lakini kwa sasa mtandao wa THRD-Coalition
unasubiri uchunguzi zaidi wa Jeshi la Polisi kwa ajili ya kutoa tamko rasmi.
Ombi letu kwa Jeshi la Polisi
 
Mtandao unalisihi Jeshi la polisi kuongeza nguvu katika uchunguzi wa mazingira na hatimaye kifo
hicho na kutoa taarifa kwa umma kuhusu kifo hichi cha mtetezi wa haki za binadamu.
Onesmo Olengurumwa,
Mratibu Wa Kitaifa
 
NI HERI KWA MTETEZI WA HAKI ZA BINADAMU KUBAKIA HAI KULIKO KUFA

No comments:

Post a Comment