Monday, December 10, 2012

BEI YA CHAKULA TABORA YAPANDA ASILIMIA 100


BEI ya chakula katika soko kuu la mjini Tabora imepanda kwa asilimia 100, na kufanya watu wenye kipato cha chini kushindwa kumudu gharama za maisha.

Uchunguzi uliofanywa, umebaini kupanda kwa bei hiyo na hivyo kupelekea wananchi wenye kipato kidogo kushindwa kabisa kumudu manunuzi hayo.

Uchunguzi huo umebaini kwamba bei hivi sasa unga wa sembe umepanda kutoka shilingi 650, hadi kufikia kuuzwa shilingi 1500 kwa kilo moja.

Aidha bei ya mchele nayo imepanda kutoka shilingi 800, ambapo kwa sasa mchele huo unauzwa shilingi 2200, wakati maharage yamepanda kutoka shilingi 900 hadi shilingi 1900, kwa kila kilo moja.

Hata hivyo Katibu wa chama cha wafanyabiashara katika soko kuu mjini Tabora Kitwana Kaswongo amesema kuwa kupanda kwa bei hityo kunatokana na kupanda kwa gharama za usafirishaji kutoka mikoa jirani ya Rukwa na mkoa mpya wa Katavi ambako hufuatwa bidhaa hiyo.

Kasongo amesema kuwa awali gunia moja la mahindi lenye uzito wa kilo 100 lilikuwa likisafirishwa kwa shilingi 8000, lakini kwa sasa gharama hiyo imepanda hadi kufikia shilingi elfu 16,000.

Amesema kwamba wafanyabiashara wengi mkoani Tabora hufuata bidhaa hiyo kutoka mikoa hiyo lakini kutoka na kupanda kwa bei ya mafuta hapa nchini, gharama hiyo imeongezeka.

Kufuatia hali hiyo Kasongo ameiomba serikali mkoani Tabora kufanya juhudi za makusudi za kuleta mahindi ili yaweze kuuzwa kwa wananchi kwa bei nafuu kwa lengo la kuwapunguzia ukali wa maisha.

Mwisho
 Na Lucas Raphael,Tabora

No comments:

Post a Comment